NEMAYAN

NEMAYAN

ROBERT

  • THE HOODS SPICK

Tuesday, November 12, 2013

MAINDA: NIMETOA MIMBA YA RAY


Stori:  Jelard Lucas
HILI ndiyo Risasi bwana! Sikia, kama ulikuwa hujui ni kwamba msanii mkongwe katika filamu za Kibongo, Ruth Suka ‘Mainda’ ameibuka na kueleza mengi ikiwemo kutoa mimba ya mpenzi wake wa siku nyingi, Vincent Kigosi, tulia hapohapo.
 
Ruth Suka ‘Mainda’.
Mbali na uhusiano wao huo uliokuwa ukifanywa siri, Mainda ameeleza kwa machungu jinsi Ray alivyomtesa kwa kumchanganya na wasanii wenzake, Blandina Chagula ‘Johari’ na Chuchu Hans ambaye ni mke wa mtu.
Risasi Mchanganyiko lilipata wasaa wa kufanya naye mahojiano ‘exculusive’ kwa saa moja na dakika tano, wikiendi iliyopita, makao makuu ya gazeti hili, Mwenge – Bamaga, jijini Dar.
Hata hivyo, alisema uhusiano wao kwa sasa umevunjika rasmi huku akibainisha jinsi alivyonyooshewa vidole na watu wakiamini kwamba aliambukizwa Ukimwi na aliyekuwa mpenzi wake kabla ya Ray, marehemu Said Maulid Banda  ‘Maxi’.
Soma mwenyewe mahojiano yalivyokuwa mstari kwa mstari, neno kwa neno:
 
Vincent Kigosi 'Ray'.
Risasi: Baada ya kifo cha Maxi, Ray alijitokeza na kukutongoza au siyo?
Mainda: Hapana, nakumbuka ilikuwa Siku ya Valentine’s Day mwaka 2004...sikumbuki kama tulitongozana ama vipi lakini ilitokea tukajikuta kwenye uhusiano.
Risasi: Umedumu kwa muda gani katika uhusiano wako na Ray?
Mainda: Miaka tisa, nilimpenda sana hata yeye alikuwa akinipenda na kuniheshimu sana.
Risasi: Kwa nini mmeachana?
Mainda: Hajaniacha wala hatujaachana. Miye ndiye nimemwacha.
Chuchu Hans.
Risasi: Jeuri ya kumuacha Ray umeitoa wapi?
Mainda: Siyo jeuri, ni kujiamini na kujitambua tu.
Risasi: Chanzo cha kumuacha nini labda?
Mainda: Nilipojihakikishia kwamba anatoka na Chuchu Hans na Johari, nikafanya uamuzi.
Risasi: Lini ulipata uhakika huo?
Mainda: Ni hivi karibuni. Niliumia sana (analia).
Risasi: Pole sana, jikaze tafadhali. Siku zote ulikuwa hujui?
Mainda: Nilikuwa nasikia tu maneno, lakini nilipothibitisha nikaamua kukaa pembeni.
Risasi: Uhusiano wako na Ray ulifikia hatua gani?
 
Blandina Chagula ‘Johari’.
Mainda: Mwaka 2009 miye na Ray tulienda kanisani kwa ajili ya kutaka kufunga ndoa. Kwa sababu  mwenzangu ni Mkatoliki ilibidi aokoke na kunifuata kwenye wokovu ili tuweze kufunga ndoa yetu, nashangaa amebadilika tena.
Risasi: Ulibadili dini kwa ajili yake?
Mainda: Big no! (Hapana kabisa) ulikuwa ni uamuzi wangu binafsi.
Risasi: Mipango yenu ya ndoa ilikuwaje?
Mainda: Tulipanga kufanya private wedding (ndoa ya siri).
Risasi: Unauzungumziaje uhusiano wako na Ray? Namaanisha ni nini hasa ambacho hakitaweza kufutika kirahisi katika kumbukumbu zako?
Mainda: Daah! (anavuta pumzi ndefu kisha anazishusha) Nilimpenda sana Ray. Ilifikia hatua nikapata mimba yake. Mapenzi yetu yakaongezeka lakini kwa bahati mbaya ilitunga nje ya kizazi na ilinitesa sana, tena kwa kuwa ilikuwa ni mimba ya kwanza sikuwa nimejitambua mapema. Madaktari wakashauri niitoe, nikakubaliana nao.
Risasi: Ilikuwa ni mwaka gani?
Mainda: Sikumbuki, ila ni kipindi tulipokuwa tukirekodi filamu iitwayo Johari (kwa kumbukumbu za Risasi ni mwaka 2005).
Risasi: Kuna madai kwamba wewe hukubaliki kwa mama yake Ray, ambaye anadaiwa anamkubali zaidi Johari, ni kweli?
Mainda: Siwezi kumsema vibaya yule mama, namheshimu sana lakini inawezekana kuna maneno ya uongo ambayo ameambiwa na watu.
Risasi: Kama yapi?
Mainda: Kuhusu miye kuwa na Ukimwi. Ngoja nikuambie kitu kaka’ngu, baada ya kifo cha Maxi, watu wengi walininyooshea vidole kwa kuamini kuwa Maxi amekufa kwa ugonjwa huo jambo ambalo siyo la kweli. Nakumbuka mwaka 2003, nilienda na Maxi Mwananyamala (Hospitali), alitolewa vipimo vingi (kikiwemo cha VVU), akabainika kuwa na kansa ya damu.
Akatakiwa kwenda Ocean Road (Hospitali) ambako walipendekeza akatwe mguu uliokuwa umeathirika na ugonjwa huo lakini alikataa. Alisema ni heri afe kwa ugonjwa huo kuliko kuzikwa akiwa na upungufu wa viungo mwilini mwake.
Risasi: Kuna tiba alishaanza kuitumia Ocean Road kabla ya kifo chake?
Mainda: Yeah! Alikuwa akichomwa mionzi, hadi kifo kilipomfika.
Risasi: Pole sana.
Mainda: Ahsante... ila baada ya kifo chake, watu wengi walihisi amekufa kwa Ukimwi na wakaamini nami pia ni mwathirika... hiyo hali ilinitesa sana (anaangua kilio).
Risasi: Pole sana, usilie...jikaze tafadhali.
Mainda: Kama kweli Maxi angekuwa amekufa kwa Ukimwi, Ray asingekubali kuwa na mimi kwa sababu  alikuwa rafiki yake na alishiriki kumuuguza kwa kiasi kikubwa.
Risasi: Kwa hiyo unaamini kwamba mama Ray alipandikizwa sumu hiyo?
Mainda: Binafsi nilikuwa simfuatilii ila mwanaye alijitahidi kuniweka karibu na mama yake.
Risasi: Kivipi?
Mainda: Mara kadhaa Ray alikuwa akinipigia simu na kunitaka niongee na mama yake au ndugu zake, aliniweka karibu sana na familia yake.
Risasi: Umewahi kupima Ukimwi?
Mainda: Siyo mara moja, baada ya maneno hayo,  mwanzo nilipima kwa hofu kwa kuhisi labda wale madaktari wa Mwananyamala walinidanganya kwa vile nilikuwa mdogo.
Risasi: Majibu yako yanasomekaje?
Mainda: Namshukuru Mungu, nipo negative (hana uambukizo).
Risasi: Ulijisikiaje ulipogundua kuwa Ray anatembea na Johari na Chuchu?
Mainda: Awali sikujua na kila nilipomuuliza Ray alinikatalia.
Risasi: Kwa hiyo ulimwamini Ray?
Mainda: Sana, tena nilipokuwa naye alikuwa akiwapigia na kuweka loud speaker kisha kuwauliza kama walikuwa wapenzi, walikataa.
Risasi: Unawachukuliaje Johari na Chuchu?
Mainda: Kwangu nawaona wapumbavu na wasiojiamini katika mapenzi. Mfano kama Ray angenipigia simu na kuniuliza kama natembea naye, ningekubali bila ya wasiwasi. Walikuwa wakijua kama miye natembea na Ray lakini kwa nini wao walifanya mapenzi yao na Ray kuwa ya siri? Mfano Chuchu alikuwa akiniita first lady na aliniambia kuwa Ray ananipenda sana, kumbe kuna kitu alikuwa akinificha.
Risasi: Chuchu alikuwa rafiki yako?
Mainda: Hapana ila alikuwa akipenda kunipigia simu na kujiaminisha kwangu kwamba alikuwa na Ray na hakuna kibaya kitakachotokea.
Risasi: Ulijuaje kama Ray anatambea na Chuchu?
Mainda: Inasikitisha kwa kweli, kwanza Chuchu ni mke wa mtu, (jina la mume kapuni) kisha amezaa na mumewe mtoto mmoja lakini anatangaza mtoto huyo ni wa Ray. Anamuweka kwenye mitandao, unadhani baba yake wa kweli anajisikiaje?
Halafu inasemekana walipokwenda Mbeya na Bongo Muvi, Chuchu alilala chumba kimoja na Ray.
Risasi: Uliambiwa na nani?
Mainda: Kuna msanii mmoja anaitwa (jina kapuni) ambaye naye alikuwa akitembea na Chuchu, ndiye aliyeshuhudia Chuchu akiingia chumbani kwa Ray. Pia ndiye aliyemfumania Chuchu na Ray Msasani hivi karibuni.
Risasi: Inadaiwa siku Ray na Chuchu walipofumaniwa, ulikuwepo na ukapandisha mashetani, ni kweli?
Mainda: Siyo kweli, sikuwepo ila siku hiyo (anamtaja jina huyo jamaa) aliniletea simu za Chuchu ambazo zilikuwa na meseji alizokuwa akichati na Ray. Halafu Chuchu ndiye mwenye tabia ya kupandisha mashetani.
Risasi: Meseji za Ray kwa Chuchu zilikuwa zinasemaje?
Mainda: Mambo ya mapenzi tu, tangu hapo niliamini kwamba Ray alikuwa akitembea na Chuchu. Nikaamua rasmi kumuacha Ray aendelee na Chura wake!
Risasi: Kwa nini unamwita Chuchu Chura?
Mainda: Wenyewe ndivyo wanavyojiita yaani ni kifupi cha Chuchu (Chu) na Ray (Ra) badala ya RJ (Ray na Johari).
Risasi: Ray alijiteteaje kwako?
Mainda: Alidai kwamba simu yake ilikuwa ikitumika na rafiki yake mwingine ambaye ni mume wa mtu (jina tunalo) akidai kwamba ndiye aliyekuwa akitembea na Chuchu lakini si kweli.
Risasi: Kama leo hii Ray akikufuata na kukuomba radhi utakubali kurudiana naye?
Mainda: Ameshaomba radhi sana, hata Chuchu alishaniomba radhi na kudai kutorudia lakini mambo ni yaleyale.
Risasi: Hebu fafanua?
Mainda: Ninaujua msururu mrefu wa wanawake wa Ray, (akaanza kuwataja majina - wamo wanenguaji na wasanii wa filamu na wengine), mmoja kwa sasa ni mke wa mtu huyo sitakutajia jina lake.
Risasi: Jambo jingine?
Mainda: Sijui kama ulisikia, Ray alipata ajali na Chura wake hivi karibuni?
Risasi: Nilisikia!
Mainda: Hiyo nayo inatosha kuthibitisha ninachokisema. Hizi zote ni laana, tukio lingine ni lile la Johari kumfumania Ray akiwa na Chura.
Risasi: Hata hilo nililisikia na liliripotiwa, vipi kuhusu Johari?
Mainda: Johari naye alikuwa akinifuatilia nyendo zangu, kuna wakati nilivaa pete ya uchumba, alihaha kutaka kujua nimevalishwa na nani?
Risasi: Alijua Ray amekuvisha?
Mainda: Nadhani!
Risasi: Ni kweli?
Mainda: Tuyaache hayo.
Risasi: Kwa nini?
Mainda: (Akionesha msisitizo) tafadhali hilo tuliache kaka.
Risasi: Uliwahi kumsaliti Ray?
Mainda: Katika maisha yangu miye ndiye huumizwa kila siku. Baada ya kuwa na Maxi mwanaume mwingine ni Ray, sikuwahi kuwa na mwingine kabla na baada ya kuwa na uhusiano naye.
Risasi: Mwanaume gani alikuingiza katika dunia ya mapenzi?
Mainda: Aaah! Sitapenda kumtaja ilikuwa kabla sijakutana na Maxi.
Risasi: Unazungumza vizuri na Johari na Chuchu?
Mainda: Sina ugomvi nao, ila sikupenda kitendo cha kuchanganywa nao kwa mwanaume mmoja. Imeniuma sana, kwa kweli sipendi kuishi mitala.
Risasi: Unaionaje Bongo Muvi baada ya miaka mitano?
Mainda: Kwanza naomba Mungu aiangamize... unafiki mwingi sana. Kuna siku nilimuuliza Ray kama yeye ndiye mwenyekiti anafanya uchafu kama huu, anaweza kumkemea msanii mwingine? Hakunijibu kitu. Mengi mabaya yanayosemwa kuhusu Bongo Muvi  ni ya kweli, tena uongozi umeoza kuanzia juu mpaka chini.
Risasi: Baada ya kuachana na Ray una mwanaume mwingine?
Mainda: Wengi wamenipigia simu kunitongoza nikawachomolea wakiwemo wasanii waliokuwa wakijua uhusiano wangu na Ray.
Risasi: Kwa nini?
Mainda: Miye huwa sitongozwi kwenye simu.
Risasi: Unatongozwaje?
Mainda: (kicheko), sikia ninaye mtu wangu lakini hatujafikia hatua ya kufanya mapenzi, tunachunguzana ili kujuana tabia kwanza.
Risasi: Ni msanii wa filamu au?
Mainda: Siyo msanii, ni mtu anayejiheshimu.
Risasi: Mara yako ya mwisho kufanya mapenzi ilikuwa lini?
Mainda: Siku chache baada ya msiba wa Albert Mangweah (msanii wa Bongo Fleva).
Risasi: Unaamini iko siku utaolewa?
Mainda: Yeah! Tena nitajifungua watoto.
Risasi: Kitu gani ambacho huwezi kukisahau maishani mwako?
Mainda: Kifo cha Kanumba na marehemu Maxi  (anaangua kilio…) vifo vyao viliniuma sana na vimeshindwa kuondoka akilini mwangu kirahisi.
Risasi: Ahsante sana kwa ushirikiano wako Mainda. Karibu tena Global Publishers.
Mainda: Nashukuru sana lakini nasema hivi; kama  Ray, Johari na Chuchu watakanusha haya niliyoyasema, nipo tayari nikutanishwe nao tena hapahapa ofisini kwenu nitazungumza mbele yao. Naahidi nitaongea mengi zaidi.
Risasi: Sawa, nashukuru sana Mainda.
Mainda: Nanyi pia… ndiyo maana nayapenda magazeti yenu.
Risasi: Kwa nini unasema hivyo?
Mainda: (Kicheko).

Sunday, November 3, 2013

HATARI!

Chanzo: Njooni Magomeni-Kimamba kuna jamaa…
Na Waandishi Wetu
HATARI! Kigogo ambaye ni mfanyabiashara jijini Dar aliyetajwa kwa jina moja la Mrema, mkazi wa Mtaa wa Kimamba, Magomeni anadaiwa kusambaza dawa za binadamu zilizokwisha muda wake ‘kueksipaya’.
Baadhi ya dawa zilizokamatwa.
CHANZO CHA HABARI
Timu ya Oparesheni Fichua Maovu (OFM) iling’atwa sikio na chanzo chake chenye maskani jirani na nyumba ya mwanaume huyo.
Chanzo: Haloo naongea na OFM?
OFM: Hapa ndipo penyewe, tukusaidie nini?
Chanzo: Njooni Magomeni-Kimamba kuna jamaa anaitwa Mrema anasambaza dawa za binadamu zilizokwisha muda wake.
OFM: Una uhakika?
Chanzo: Ninyi njooni mfanye kazi yenu na kama mimi ni muongo nifanyeni chochote.
OFM: Oke tuachie kazi.
Askari akikagua dawa zilizokamatwa.
OFM KAZINI
Ikiwa inarandaranda eneo la tukio, OFM ilitonywa kuwa Mrema na mkewe wamekuwa wakijihusisha na biashara hatari ya kununua dawa za binadamu zilizokwisha muda wake kwa matumizi ya binadamu kisha kuzipaki upya na kuwauzia wenye famasi wanaokula nao dili.
Ilisemekana kuwa dawa hizo ni zile zinazotupwa dampo tayari kwa kuteketezwa, Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar.
Ilidaiwa kuwa wakishakula dili huko dampo na kuzipata, huzipaki upya katika makopo mengine na kuziuza famasi kwa bei ya chini kidogo ukilinganisha na bei halali.
Ilielezwa kuwa jamaa huyo na mkewe kila baada ya wiki moja huwa wanashusha mzigo wa dawa hizo usiku wa manane kisha kupaki na kuziuza bila kujali kuwa ni hatari na wanafanya mauaji kwa raia wasiokuwa na hatia.
Madawa aliyokutwa nayo mtuhumiwa.
POLISI
Baada ya kujiridhisha kuwa ni kweli kuna biashara hiyo haramu nyumbani kwa Mrema, OFM iliwataarifu polisi wa doria Magomeni.
Hata hivyo, wakati kikosi kazi ‘kinaliteka’ eneo la tukio, Mrema na mkewe walifanikiwa kutoroka kupitia mlango wa nyuma.
UKAGUZI
Timu hiyo ilimuomba kijana aliyekutwa nyumbani hapo ruhusa ya kuingia ndani ili kukagua kama kuna kitu kama hicho ndipo mambo yakabumburuka kwani mzigo wa dawa mbalimbali ulikutwa ndani.
Walifanikiwa kukuta maboksi mengi ya dawa za binadamu za aina mbalimbali na makopo tupu ambayo hutumika kuwekea dawa hizo.
Mbali na dawa hizo, kulikuwa na lebo nyingi za kutengeneza zilizoonesha muda wa dawa hizo kwisha muda wake kwa kutumia sampo ya zile za halali.
KIJANA AKIRI
Kijana aliyekutwa ambaye alieleza kuwa ni mfanyakazi anayemsaidia Mrema, alikiri mabosi wake hao kufanya biashara hiyo ya dawa ambazo zimepitwa muda wake.
Pia alikiri kuwa kazi ya kupaki dawa hizo hufanyika usiku mnene ili dili lisivuje.
“Mkinikamata mimi mtanionea tu ni baba na mama ndiyo wanafanya kazi hiyo tena huwa wanaifanya usiku wa manane na kuziuza katika maduka ya madawa,” alisema kijana huyo.
PATROO
Hata hivyo, OFM na polisi walizunguka maeneo hayo wakifanya ‘patroo’ kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi 4:30 usiku lakini Mrema na mkewe hawakuonekana.
Baadhi ya dawa zilizokwisha muda wake zilizokutwa nyumbani kwa Mrema ni pamoja na Penizen-V, Artefan 20/120, Amoxicillin, Antibiotics, dawa za sindano na nyingine nyingi.
WAZIRI MWINYI
Juhudi za kumpata Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani.
TFDA WANASEMAJE?
Hata hivyo, Ijumaa Wikienda lilizungumza na Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza ambaye alifafanua ni kwa jinsi gani kunakuwa na usimamizi wa hali ya juu katika uteketezaji wa dawa zilizokwisha muda wake.
Alisema kuwa zoezi hilo linapofanyika linahusisha mamlaka zipatazo tano kama polisi, Mamlaka ya Mapato (TRA), manispaa au halmashauri, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na TFDA wenyewe.
Hata hivyo, alishukuru kwa kumjulisha juu ya tukio hilo na kuahidi mamlaka hiyo kulifanyia kazi mara moja.
MASHUHUDA
Wakizungumzia tukio hilo baada ya dawa hizo kukamatwa, mashuhuda walidai kuwa kitendo hicho ni kucheza na maisha ya binadamu.
“Wapo watu wameshakunywa hizi dawa wakijua watapona lakini utakuta wanakufa kwa sababu badala ya kutibu wanaongeza matatizo mengine tena makubwa.
“Hapa kinachotakiwa ili kunusuru watu ni mamlaka husika kuhakikisha zinafanya ukaguzi wa hizi famasi kuondoa tatizo hili kubwa,” alisema Laizer, mkazi wa Magomeni, Dar.
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni wawili hao walikuwa wakisakwa na polisi ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

SHAROBARO ALA KICHAPO KISA MKE WA MTU


Issa Mnally Na Richard Bukos
KIJANA mmoja mtanashati ‘Sharobaro’ ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja juzikati alijikuta akichezea kichapo cha mbwa mwizi kisa kikidaiwa kuwa ni mke wa mtu.

Usione vyaelea: Sharobaro (katikati) akilia baada ya kuchezea kichapo kwa kukutwa na mke wa mtu.
Tukio hilo lilijiri saa saba usiku mwishoni mwa wiki iliyopita, Chalinze mkoani Pwani ambapo mapaparazi wetu walikwenda kwa ajili ya uzinduzi wa kundi jipya la sanaa liitwalo 3 Ways.
Wakati shamrashamra zikiendelea, ghafla liliibuka timbwili na katika kufuatilia ilibainika sharobaro anayeishi eneo hilo alikuwa akila kipigo kutoka kwa mwanaume mmoja akimtuhumu kuwa alimkuta akiwa amekaa chobingo kihasarahasara na mkewe.

Mke wa mtu sumu: Sharobaro hoi baada ya kipigo.
Licha ya baadhi ya wasanii kujaribu kuingilia kati ugomvi huo, jamaa huyo aliendelea kushusha kichapo hadi pale watu walipomtolea uvivu na kumzuia asije akasababisha mauaji.
“Unajifanya sharobaro halafu unazengea wake za watu, sasa wee umeipata fresh na huyo mwenzako akirudi nyumbani naye
atakiona,” alisikika akisema mwanaume huyo huku akionekana kufura.
Kufuatia kichapo hicho, sharobaro huyo alijikuta akiangua kilio huku akilalama kuwa mwanamke huyo amemponza na kumharibia siku yake.

Kilio: Sharobaro akizidi kububujikwa na machozi baada ya kipondo kutoka kwa mwenye mali.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda walisema, kipigo alichopata kijana huyo ni fundisho kwa masharobaro wengine ambao wamekuwa na uhusiano wa karibu na wake za watu.
“Unajua hawa vijana hii ndiyo dawa yao, wanajisahau sana. Yaani anajua kabisa fulani ni mke wa mtu lakini anajiweka, sasa kwa kipigo hiki atakuwa fundisho,” alisema baba mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Baba Zulfa.
Aidha, wengine walimtetea kijana huyo na kudai kuwa mwanamke huyo ndiye anayestahili kulaumiwa kwa kukubali kukaa gizani na kijana huyo wakati akijua ni mke wa mtu.

Tuesday, June 18, 2013

Breaking News:Mapambano makali Arusha,Lema amenusurika kufa

Watu waliolipuliwa na bomu katika mkutano wa Chadema jijini Arusha hivi karibuni wakiwa wamelala chini               Arusha Tanzania
HALI tete katika jijini la Arusha muda huu,Polisi wanapiga mabomu ovyo,watu waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Soweto wakisubiri kuaga miili ya watu waliofariki dunia katika shambulio la kigaidi wametawanywa kwa mabomu.
Mbali na watu kutawanywa kwa mabomu hayo,Mbunge wa Arusha Mjini Godless Lema menusurika kufa huku gari lake likiharibiwa vibaya mabomu ya Polisi .
Mwandishi wa Habarimpya.com akiwa eneo la tukio ameshuhudia majeruhi kibao wakikimbizwa katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.
Barabara kuu ya kuingia mjini imefungwa, mabomu yanapigwa kila kona jijini Arusha Risasi za moto zinatumika.
Akizungumza na Habaimpya.com katika eneo la tukio mmoja wa wahanga wa tukio hilo, Agnes Mosha anasema kwamba hajui walipo ndugu zake wawili waliokuwa katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuaga miili ya rafiki zao.
"Dada nisaidie nivuke barabara nikimbie Mount Meru nasikia kuna dada yangu amepigwa bomu na hali yake ni mbaya sana,siwezi kuvuka dada sina nguvu tena jamani"alilalamika Agnes mbele ya Mwandishi wa Habarimpya.com kisha akapoteza fahamu na kuanguka chini.
Hata hivyo baada ya Agnes kuanguka chini hakuweza kuinuka huku watu wakikimbia na kumkanyaga,kulingana na hali kuwa mbaya eneo hilo mwandishi wa Habarimpya.com pia alilazimika kukimbia nakutafuta eneo la kujificha.

Monday, June 17, 2013

SIRI ZAIDI KIFO CHA MWANAMUZIKI LANGA!

Na Mwandishi Wetu
MWILI wa mwanamuziki Langa Kileo jana (Jumatatu) ulipumzishwa kwenye nyumba ya milele katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar lakini nyuma ya kifo chake kuna siri ambayo rafiki yake wa karibu (jina linahifadhiwa) mkazi wa Mikocheni A jijini Dar ameamua kuiweka hadharani.
Akizungumza na Uwazi juzi, rafiki huyo wa marehemu alisema, siku chache kabla ya kifo chake alimfuata na kumwambia kuwa Israel mtoa roho anamtembelea usiku na anahisi siku si nyingi atamfuata mshikaji wake aliyetangulia mbele ya haki, Albert Mangweha ‘Ngwea’.
“Hii ni siri ambayo hata ndugu zake hawaijui lakini mshikaji alijua anakufa. Alijitahidi kukikwepa kifo lakini alishindwa. Siku chache kabla hajafa, usiku alikuja kwangu na kuniambia kule kwao kwenye geto lake analoishi ambalo liko ghorofani, anaona mauzauza na anahisi kifo kinamuita.
“Nilishangazwa sana na maneno yale. Akazidi kuniambia eti kwa jinsi mambo yanavyokwenda hawezi kuendelea kulala kwao na kuanzia siku ile angelala na  mshikaji wetu mwingine pale Geza, Mikocheni A.
“Kweli siku hiyo alilala pale akiwa na hofu kubwa na asubuhi baadhi ya watu wakawa wanamshangaa akiwa ‘amezima’ nje ya lile geto la mshikaji wake. Alivyoondoka sikumuona tena mpaka nilipokuja kuambiwa yuko hoi kwa malaria na kesho yake nikasikia hatunaye, nimeumia sana,” alisema mtoa habari huyo.
Alipoulizwa juu ya uhusiano wa kifo cha Langa na matumizi ya madawa ya kulevya, rafiki huyo alisema: “Inaweza ikawa ngumu kwa ndugu wa marehemu kuhusisha kifo chake na madawa ya kulevya lakini mimi namjua Langa nje ndani, ukweli ni kwamba jamaa alikuwa akiendelea kula ‘mambo’.
“Alikuwa anakuja maskani tunakula mambo yetu na hata wakati anafanya kazi kwenye ile Kampuni ya Barrick hapa Dar, ilikuwa kabla hajaenda anapita kwanza huku uswahilini kisha ndiyo anaenda. Kwa maana hiyo malaria ndiyo iliyomuua lakini hata madawa yamechangia.”
Langa alifariki dunia Juni 13, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amini!

BOMU ARUSHA... NJAMA NZITO

Na Joseph Ngilisho, Arusha
NYUMA ya matukio ya kigaidi ambayo yamefululiza kutokea jijini Arusha kuna njama nzito baada ya kuibuka maswali mengi yanayosababisha mahali hapa kutokuwa shwari na salama kufuatia bomu lililolipuliwa Jumamosi iliyopita, Uwazi lina uchambuzi.
Bomu hilo lililipuliwa katika mkutano wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kaloleni jijini hapa na kusababisha kuvunjika ghafla huku likiua watu wawili na wengine zaidi ya sitini kujeruhiwa.
Mlipuaji alilipua bomu hilo saa 11:50: jioni, dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe (pichani) kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto jijini hapa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kisha kuacha maswali mengi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliwataja waliofariki kuwa ni Judith William Mushi (46) ambaye alikuwa Katibu Kata wa Chadema, Kata ya Sokoni One na mkazi wa eneo hilo aliyemtaja kwa jina moja la Justine (16), mkazi wa Sombetini ambaye alifariki katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Tukio hilo ni la pili la bomu kulipuliwa katika mkusanyiko wa watu kwani Mei 5, mwaka huu bomu lililipuliwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti jijini hapa na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.

JE, LILIMLENGA MBOWE?
Baadhi ya wanachama wa Chadema waliozungumza na Uwazi walidai kuwa bomu hilo la kurusha kwa mkono lililenga kumuua Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutokana na sababu za kisiasa.
Wachunguzi walijiuliza kama mlipuaji alikuwa na nia ya  kumuua Mbowe na Lema kwa nini alitupa bomu kwa wananchi wakati viongozi hao walikuwa wanaonekana wakikusanya michango ya fedha kuchangia ununuzi wa maji kwa wasimamizi wao wa uchaguzi ulioahirishwa?
Pia swali lingine, kama hivyo ndivyo, kwa nini mlipuaji alirusha bomu wakati ambao Mbowe na Lema walikuwa wameshuka jukwaani?

CHADEMA WALIJIPIGA BOMU WENYEWE?
Wapo waliodai kuwa hujuma hizo ni mbinu za kisiasa zinazofanywa na wanasiasa wenye ufinyu wa mawazo huku wakijiuliza Chadema wanahusika?
Swali hilo lilijibiwa na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wakidai kuwa hawawezi kuhusika kutokana na ukweli kwamba hata kiongozi wao, Judith ameuawa na bomu hilo.

MRUSHA BOMU ALIOKOKAJE?
Watu mbalimbali wanajiuliza kama mrusha bomu alikuwa karibu na umati, aliwezaje kufanya unyama huo bila kukamatwa na wananchi waliomuona akirusha?
Pia katika mkutano huo kulikuwa na ulinzi wa polisi waliokuwa wakilinda usalama wa raia, ilikuwaje mrusha bomu huyo ambaye hakukamatwa, akaweza kuwatoroka hata wao (polisi)?

MLIPUAJI BOMU ANATAKA SERIKALI ICHUKIWE?
Wapo waliodai kuwa kama mrusha bomu yupo nje ya siasa, basi zinazofanyika ni njama nzito za kuwagombanisha wananchi na serikali yao ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kitu ambacho serikali inapaswa kufanyia kazi.
“Kuna uwezekano labda ni haya makundi ya kigaidi na waasi kama M-23 na Al-Shaabab yanayolenga kuzivuruga serikali za Afrika Mashariki kwa kuzichonganisha na wananchi wake,” alisema Mzee Minja, kada wa Chadema mjini hapa.
Baadhi ya wananchi walisema mlipuaji alilenga kuua watu wengi na matokeo yake ni kwamba licha ya watu hao wawili kufariki dunia, majeruhi waliolazwa katika hospitali mbalimbali jijini hapa na KCMC mkoani Kilimanjaro, idadi iliyothibitishwa na polisi imefikia 60.
Habari zilieleza kuwa majeruhi wanne, hali zao zilikuwa mbaya huku mtoto, Farad Jamal (7), akiwa katika hali mbaya zaidi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya KCMC.
Mbowe amesema “ tukio hili ni kubwa na lina mambo mengi, chama kitawahudumia majeruhi wote.”
Kufuatia tukio hilo, msimamizi wa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne, Jimbo la Arusha, Sipora Liana ambaye ni mkurugenzi wa jiji, alitangaza kuahirisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike juzi (Jumapili) hadi Juni 30, mwaka huu.
Liana alisema kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni kutokana na hali tete iliyojitokeza Jumamosi na kusababisha uvunjifu wa amani hivyo kwa mtazamo huo usingeweza kufanyika kutokana na hali ya usalama kuwa mdogo.
Mkuu wa Mkoa, Mulongo alisema kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo na aliwasihi wananchi waendelee na shughuli zao wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

MAJERUHI WAZUNGUMZA
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Seliani, Abdalah Alila (39) alisema kuwa akiwa katika mkutano huo majira ya saa 11.50 jioni, aliona kitu cheusi kikidondoka karibu yake na baadaye alisikia kishindo kizito.
“Ghafla nilijikuta chini na damu zikinichuruzika huku nikishindwa kutembea, nikatambaa kuomba msaada kwa watu waliokuwa wakikimbia hovyo,” alisema.

MRUSHA BOMU
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto, hali iliyozidisha vurugu.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za Jiji la Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia hovyo.
Kitendo cha watu kukimbia hovyo kuliwafanya polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi, hali ambayo ilizidisha taharuki.

BADO HOFU IMETANDA
Pamoja na viongozi kujitahidi kutuliza wananchi lakini bado hali ni tete jijini hapa kwa kuwa watu wana hofu hasa maeneo ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi huku wengine wakijitahidi muda mwingi kuwa majumbani mwao.
Wananchi waliozungumza na Uwazi kwa nyakati tofauti kuhusu tukio hilo, wamemuomba Rais Kikwete kufuatilia kwa kina matukio hayo ili maswali yote yanayoulizwa hivi sasa yaweze kujibiwa japokuwa tayari amesema  serikali itafanya kila liwezekanalo kuwasaka waliohusika na kitendo hicho ili washitakiwe.