MAISHA
yakaendelea, Khalid hakuwa mtu mwenye pesa nyingi lakini aliamua
kutumia akiba yake kuhakikisha Gift anakuwa na furaha, anatimiza pia
ndoto zake. Khalid alieleza ombi lake la kumtaka wawe na uhusiano wa
kimapenzi na panapo majaliwa, waweze kufunga ndoa.
Gift
ombi hilo alilikubali. Wiki moja baadaye, Khalid alimsafirisha Gift kwa
ndege kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia nafasi za kujiunga
na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Gift
kusafiri kwa ndege, aliona ndoto, akamshukuru sana Khalid.
Alipata
chuo, Khalid akamlipia ada, bweni na matumizi mengine. Kwa kifupi Khalid
aligeuka baba kwa Gift, alimhudumia kila kitu. Gift alipopatwa na
tatizo lolote, mtu wa kwanza kumpigia alikuwa ni Khalid ambaye alitatua
bila kusita, akijua anajenga maisha ya mkewe mtarajiwa.
Kuna wakati
ubinadamu ulimuingia Khalid, akawa anaomba kufanya mapenzi na Gift
lakini hakufanikiwa. Siku zote Gift alimwambia asubiri mpaka
watakapofunga ndoa. Japo Khalid ilimuuma lakini upande mwingine aliona
msimamo wa Gift ni mzuri na alilegea kila alipokumbuka kauli tamu ya
Gift: “Usijali mpenzi wangu, mimi ni wako, tutafanya mpaka utachoka.”
Siku,
wiki, miezi, ikawa mwaka, miaka ikapita, Gift akamaliza chuo. Hakutaka
hata kurudi Mwanza. Alichokikataa ni kuonana na Khalid. Alimuona
mwanaume asiye na elimu, kwa hiyo kuwa na mume aina yake aliona kama ni
kupoteza dira ya maisha. Wanaume wasomi ni wengi.
Khalid alijitahidi
kufika Dar es Salaam, akaa mwezi mzima bila kuonana na Gift ambaye kwa
kuona kero, akaamua kubadili na namba ya simu. Kutokana na uhusiano wao
kutambuliwa mpaka na wazazi pamoja na ndugu wengine, aliwashirikisha
lakini hakuna alichoambulia.
Sabrina ni rafiki yake Gift, akaamua
kuingilia kati, kumshauri Gift atambue umuhimu wa Khalid kwa sababu pale
alipo asingefika kama siyo mwanaume huyo lakini ushauri huo ulionekana
sawa na takataka: “Sikiliza Sabrina, mimi ni msomi, daktari, natakiwa
niwe na mwanaume msomi mwenzangu.”
Akaendelea: “Nilikuwa na Khalid
kwa sababu alijipendekeza kwangu na alionesha anao uwezo wa kunisaidia.
Nisingeweza kuacha hiyo nafasi lakini sasa hivi nimefanikiwa, Khalid
kwangu wa nini tena? Ataniharibia tu maisha yangu. Lazima niyatengeneze
maisha yangu kisomi.”
Gift alipoona msimamo wa Sabrina kwa Khalid
umekuwa mkali, akimsisitiza anachokifanya siyo kizuri, alimjibu: “Hivi
Sabrina, na wewe si mwanamke? Kama unamuona Khalid ni mwanaume wa maana
sana, si uende akakuoe wewe? Tusisumbuane, kwanza yule siyo mwanaume
wangu, sijawahi kutembea naye.”
Khalid alilia, machozi yakakauka,
akaamua kuongeza juhudi kwenye biashara zake. Hatua zilikuwa ndefu na
mafanikio yaliendelea kwa Khalid. Akafanikiwa kuanzisha maduka ya nguo,
Dar es Salaam, Mwanza na Arusha. Vilevile akaanzisha biashara mbalimbali
ambazo zilimfanya kuwa anasafiri kwenda nchi mbalimbali.
Kutokana na
historia yake ya kukosa mke kwa sababu ya elimu, aliamua kutumia
utajiri wake kuanzisha mfuko kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa kiume
kujiendeleza kielimu. Alifanya mambo mengi makubwa, ikiwemo kujenga
majumba ambayo baadhi aliyafanya kuwa ofisi zake kwa ajili ya kuratibu
biashara zake.
Khalid alipotaka kufunga ndoa, akamuona Sabrina ndiyo
mke sahihi kwake. Japo mwanzoni ilikuwa ngumu kueleweka lakini baadaye
kilieleweka. Gift aliposikia Sabrina na Khalid wamefunga ndoa, moyo
ukamuuma sana, aliumia zaidi kwa sababu wanaume wasomi aliowataka
walimtesa sana.
Hata hivyo, hiyo haikumuuma kama siku alipoomba kazi
kwenye hospitali binafsi inayoitwa KS Health Centre bila kujua
inamilikiwa na nani. Siku anaitwa kwenye usaili ndipo aliposhtuka,
kugundua kwamba hospitali hiyo ni ya Khalid lakini inasimamiwa na mkewe
(Sabrina) ambaye naye ni daktari.
Gift baada ya kufanyiwa usaili,
aliondoka kichwa kikiwa kizito. Wakati yeye alikwenda kwenye usaili
akiwa na taksi na kuondoka kwa taksi, kwa macho yake alimshuhudia
Sabrina anaendesha gari la kifahari aina ya BMW X6 rangi ya chungwa.
Kwa
haraka, Gift akaingiwa na mawazo kwamba kumbe maisha ya raha aliyonayo
Sabrina, yangekuwa yake kama asingemdharau Khalid. Alimuona ni kijana
aliyeishia kidato cha nne lakini ameweza kufanya mambo makubwa
kumuwezesha kumiliki pesa na mali nyingi.
Mfano wangu una maana kuwa
Gift ni mnyonyaji, alimuona Khalid ni daraja la kutimiza malengo yake
kimaisha bila kuzingatia kwamba Khalid naye ni binadam. Kumbe badala ya
kumfanyia visa, kumnynyasa, kumsimanga na kumdhalilisha kielimu,
angeweza kushirikiana naye kujenga maisha bora.
Ingependeza kama Gift
angeona umuhimu wa kutumia elimu yake kushirikiana na Khalid kujenga
maisha lakini kwa sababu aliingiwa na ubinafsi, dharau kwa kumuona ni
mwaume mbumbumbu, ndiyo maana baadaye akajuta. Ni sawa na mtu
anayekumbuka almasi aliyoitupa, wakati akiwa bize anakusanya mawe.
Hakuna
sababu ya kujuta baadaye, wala haitakiwa kuachana kisa mmoja amemuona
mwenzake mnyonyaji, isipokuwa kila mmoja anapaswa kujiuliza na kupata
jibu: “Ninapewa, je mimi natoa nini kwa mwenzangu?”