NEMAYAN

NEMAYAN

ROBERT

  • THE HOODS SPICK

Tuesday, June 18, 2013

Breaking News:Mapambano makali Arusha,Lema amenusurika kufa

Watu waliolipuliwa na bomu katika mkutano wa Chadema jijini Arusha hivi karibuni wakiwa wamelala chini               Arusha Tanzania
HALI tete katika jijini la Arusha muda huu,Polisi wanapiga mabomu ovyo,watu waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Soweto wakisubiri kuaga miili ya watu waliofariki dunia katika shambulio la kigaidi wametawanywa kwa mabomu.
Mbali na watu kutawanywa kwa mabomu hayo,Mbunge wa Arusha Mjini Godless Lema menusurika kufa huku gari lake likiharibiwa vibaya mabomu ya Polisi .
Mwandishi wa Habarimpya.com akiwa eneo la tukio ameshuhudia majeruhi kibao wakikimbizwa katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.
Barabara kuu ya kuingia mjini imefungwa, mabomu yanapigwa kila kona jijini Arusha Risasi za moto zinatumika.
Akizungumza na Habaimpya.com katika eneo la tukio mmoja wa wahanga wa tukio hilo, Agnes Mosha anasema kwamba hajui walipo ndugu zake wawili waliokuwa katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuaga miili ya rafiki zao.
"Dada nisaidie nivuke barabara nikimbie Mount Meru nasikia kuna dada yangu amepigwa bomu na hali yake ni mbaya sana,siwezi kuvuka dada sina nguvu tena jamani"alilalamika Agnes mbele ya Mwandishi wa Habarimpya.com kisha akapoteza fahamu na kuanguka chini.
Hata hivyo baada ya Agnes kuanguka chini hakuweza kuinuka huku watu wakikimbia na kumkanyaga,kulingana na hali kuwa mbaya eneo hilo mwandishi wa Habarimpya.com pia alilazimika kukimbia nakutafuta eneo la kujificha.

Monday, June 17, 2013

SIRI ZAIDI KIFO CHA MWANAMUZIKI LANGA!

Na Mwandishi Wetu
MWILI wa mwanamuziki Langa Kileo jana (Jumatatu) ulipumzishwa kwenye nyumba ya milele katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar lakini nyuma ya kifo chake kuna siri ambayo rafiki yake wa karibu (jina linahifadhiwa) mkazi wa Mikocheni A jijini Dar ameamua kuiweka hadharani.
Akizungumza na Uwazi juzi, rafiki huyo wa marehemu alisema, siku chache kabla ya kifo chake alimfuata na kumwambia kuwa Israel mtoa roho anamtembelea usiku na anahisi siku si nyingi atamfuata mshikaji wake aliyetangulia mbele ya haki, Albert Mangweha ‘Ngwea’.
“Hii ni siri ambayo hata ndugu zake hawaijui lakini mshikaji alijua anakufa. Alijitahidi kukikwepa kifo lakini alishindwa. Siku chache kabla hajafa, usiku alikuja kwangu na kuniambia kule kwao kwenye geto lake analoishi ambalo liko ghorofani, anaona mauzauza na anahisi kifo kinamuita.
“Nilishangazwa sana na maneno yale. Akazidi kuniambia eti kwa jinsi mambo yanavyokwenda hawezi kuendelea kulala kwao na kuanzia siku ile angelala na  mshikaji wetu mwingine pale Geza, Mikocheni A.
“Kweli siku hiyo alilala pale akiwa na hofu kubwa na asubuhi baadhi ya watu wakawa wanamshangaa akiwa ‘amezima’ nje ya lile geto la mshikaji wake. Alivyoondoka sikumuona tena mpaka nilipokuja kuambiwa yuko hoi kwa malaria na kesho yake nikasikia hatunaye, nimeumia sana,” alisema mtoa habari huyo.
Alipoulizwa juu ya uhusiano wa kifo cha Langa na matumizi ya madawa ya kulevya, rafiki huyo alisema: “Inaweza ikawa ngumu kwa ndugu wa marehemu kuhusisha kifo chake na madawa ya kulevya lakini mimi namjua Langa nje ndani, ukweli ni kwamba jamaa alikuwa akiendelea kula ‘mambo’.
“Alikuwa anakuja maskani tunakula mambo yetu na hata wakati anafanya kazi kwenye ile Kampuni ya Barrick hapa Dar, ilikuwa kabla hajaenda anapita kwanza huku uswahilini kisha ndiyo anaenda. Kwa maana hiyo malaria ndiyo iliyomuua lakini hata madawa yamechangia.”
Langa alifariki dunia Juni 13, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amini!

BOMU ARUSHA... NJAMA NZITO

Na Joseph Ngilisho, Arusha
NYUMA ya matukio ya kigaidi ambayo yamefululiza kutokea jijini Arusha kuna njama nzito baada ya kuibuka maswali mengi yanayosababisha mahali hapa kutokuwa shwari na salama kufuatia bomu lililolipuliwa Jumamosi iliyopita, Uwazi lina uchambuzi.
Bomu hilo lililipuliwa katika mkutano wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kaloleni jijini hapa na kusababisha kuvunjika ghafla huku likiua watu wawili na wengine zaidi ya sitini kujeruhiwa.
Mlipuaji alilipua bomu hilo saa 11:50: jioni, dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe (pichani) kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto jijini hapa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kisha kuacha maswali mengi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliwataja waliofariki kuwa ni Judith William Mushi (46) ambaye alikuwa Katibu Kata wa Chadema, Kata ya Sokoni One na mkazi wa eneo hilo aliyemtaja kwa jina moja la Justine (16), mkazi wa Sombetini ambaye alifariki katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Tukio hilo ni la pili la bomu kulipuliwa katika mkusanyiko wa watu kwani Mei 5, mwaka huu bomu lililipuliwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti jijini hapa na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.

JE, LILIMLENGA MBOWE?
Baadhi ya wanachama wa Chadema waliozungumza na Uwazi walidai kuwa bomu hilo la kurusha kwa mkono lililenga kumuua Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutokana na sababu za kisiasa.
Wachunguzi walijiuliza kama mlipuaji alikuwa na nia ya  kumuua Mbowe na Lema kwa nini alitupa bomu kwa wananchi wakati viongozi hao walikuwa wanaonekana wakikusanya michango ya fedha kuchangia ununuzi wa maji kwa wasimamizi wao wa uchaguzi ulioahirishwa?
Pia swali lingine, kama hivyo ndivyo, kwa nini mlipuaji alirusha bomu wakati ambao Mbowe na Lema walikuwa wameshuka jukwaani?

CHADEMA WALIJIPIGA BOMU WENYEWE?
Wapo waliodai kuwa hujuma hizo ni mbinu za kisiasa zinazofanywa na wanasiasa wenye ufinyu wa mawazo huku wakijiuliza Chadema wanahusika?
Swali hilo lilijibiwa na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wakidai kuwa hawawezi kuhusika kutokana na ukweli kwamba hata kiongozi wao, Judith ameuawa na bomu hilo.

MRUSHA BOMU ALIOKOKAJE?
Watu mbalimbali wanajiuliza kama mrusha bomu alikuwa karibu na umati, aliwezaje kufanya unyama huo bila kukamatwa na wananchi waliomuona akirusha?
Pia katika mkutano huo kulikuwa na ulinzi wa polisi waliokuwa wakilinda usalama wa raia, ilikuwaje mrusha bomu huyo ambaye hakukamatwa, akaweza kuwatoroka hata wao (polisi)?

MLIPUAJI BOMU ANATAKA SERIKALI ICHUKIWE?
Wapo waliodai kuwa kama mrusha bomu yupo nje ya siasa, basi zinazofanyika ni njama nzito za kuwagombanisha wananchi na serikali yao ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kitu ambacho serikali inapaswa kufanyia kazi.
“Kuna uwezekano labda ni haya makundi ya kigaidi na waasi kama M-23 na Al-Shaabab yanayolenga kuzivuruga serikali za Afrika Mashariki kwa kuzichonganisha na wananchi wake,” alisema Mzee Minja, kada wa Chadema mjini hapa.
Baadhi ya wananchi walisema mlipuaji alilenga kuua watu wengi na matokeo yake ni kwamba licha ya watu hao wawili kufariki dunia, majeruhi waliolazwa katika hospitali mbalimbali jijini hapa na KCMC mkoani Kilimanjaro, idadi iliyothibitishwa na polisi imefikia 60.
Habari zilieleza kuwa majeruhi wanne, hali zao zilikuwa mbaya huku mtoto, Farad Jamal (7), akiwa katika hali mbaya zaidi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya KCMC.
Mbowe amesema “ tukio hili ni kubwa na lina mambo mengi, chama kitawahudumia majeruhi wote.”
Kufuatia tukio hilo, msimamizi wa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne, Jimbo la Arusha, Sipora Liana ambaye ni mkurugenzi wa jiji, alitangaza kuahirisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike juzi (Jumapili) hadi Juni 30, mwaka huu.
Liana alisema kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni kutokana na hali tete iliyojitokeza Jumamosi na kusababisha uvunjifu wa amani hivyo kwa mtazamo huo usingeweza kufanyika kutokana na hali ya usalama kuwa mdogo.
Mkuu wa Mkoa, Mulongo alisema kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo na aliwasihi wananchi waendelee na shughuli zao wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

MAJERUHI WAZUNGUMZA
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Seliani, Abdalah Alila (39) alisema kuwa akiwa katika mkutano huo majira ya saa 11.50 jioni, aliona kitu cheusi kikidondoka karibu yake na baadaye alisikia kishindo kizito.
“Ghafla nilijikuta chini na damu zikinichuruzika huku nikishindwa kutembea, nikatambaa kuomba msaada kwa watu waliokuwa wakikimbia hovyo,” alisema.

MRUSHA BOMU
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto, hali iliyozidisha vurugu.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za Jiji la Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia hovyo.
Kitendo cha watu kukimbia hovyo kuliwafanya polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi, hali ambayo ilizidisha taharuki.

BADO HOFU IMETANDA
Pamoja na viongozi kujitahidi kutuliza wananchi lakini bado hali ni tete jijini hapa kwa kuwa watu wana hofu hasa maeneo ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi huku wengine wakijitahidi muda mwingi kuwa majumbani mwao.
Wananchi waliozungumza na Uwazi kwa nyakati tofauti kuhusu tukio hilo, wamemuomba Rais Kikwete kufuatilia kwa kina matukio hayo ili maswali yote yanayoulizwa hivi sasa yaweze kujibiwa japokuwa tayari amesema  serikali itafanya kila liwezekanalo kuwasaka waliohusika na kitendo hicho ili washitakiwe.