NEMAYAN

NEMAYAN

ROBERT

  • THE HOODS SPICK

Monday, June 17, 2013

BOMU ARUSHA... NJAMA NZITO

Na Joseph Ngilisho, Arusha
NYUMA ya matukio ya kigaidi ambayo yamefululiza kutokea jijini Arusha kuna njama nzito baada ya kuibuka maswali mengi yanayosababisha mahali hapa kutokuwa shwari na salama kufuatia bomu lililolipuliwa Jumamosi iliyopita, Uwazi lina uchambuzi.
Bomu hilo lililipuliwa katika mkutano wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kaloleni jijini hapa na kusababisha kuvunjika ghafla huku likiua watu wawili na wengine zaidi ya sitini kujeruhiwa.
Mlipuaji alilipua bomu hilo saa 11:50: jioni, dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe (pichani) kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto jijini hapa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kisha kuacha maswali mengi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliwataja waliofariki kuwa ni Judith William Mushi (46) ambaye alikuwa Katibu Kata wa Chadema, Kata ya Sokoni One na mkazi wa eneo hilo aliyemtaja kwa jina moja la Justine (16), mkazi wa Sombetini ambaye alifariki katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Tukio hilo ni la pili la bomu kulipuliwa katika mkusanyiko wa watu kwani Mei 5, mwaka huu bomu lililipuliwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti jijini hapa na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.

JE, LILIMLENGA MBOWE?
Baadhi ya wanachama wa Chadema waliozungumza na Uwazi walidai kuwa bomu hilo la kurusha kwa mkono lililenga kumuua Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutokana na sababu za kisiasa.
Wachunguzi walijiuliza kama mlipuaji alikuwa na nia ya  kumuua Mbowe na Lema kwa nini alitupa bomu kwa wananchi wakati viongozi hao walikuwa wanaonekana wakikusanya michango ya fedha kuchangia ununuzi wa maji kwa wasimamizi wao wa uchaguzi ulioahirishwa?
Pia swali lingine, kama hivyo ndivyo, kwa nini mlipuaji alirusha bomu wakati ambao Mbowe na Lema walikuwa wameshuka jukwaani?

CHADEMA WALIJIPIGA BOMU WENYEWE?
Wapo waliodai kuwa hujuma hizo ni mbinu za kisiasa zinazofanywa na wanasiasa wenye ufinyu wa mawazo huku wakijiuliza Chadema wanahusika?
Swali hilo lilijibiwa na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wakidai kuwa hawawezi kuhusika kutokana na ukweli kwamba hata kiongozi wao, Judith ameuawa na bomu hilo.

MRUSHA BOMU ALIOKOKAJE?
Watu mbalimbali wanajiuliza kama mrusha bomu alikuwa karibu na umati, aliwezaje kufanya unyama huo bila kukamatwa na wananchi waliomuona akirusha?
Pia katika mkutano huo kulikuwa na ulinzi wa polisi waliokuwa wakilinda usalama wa raia, ilikuwaje mrusha bomu huyo ambaye hakukamatwa, akaweza kuwatoroka hata wao (polisi)?

MLIPUAJI BOMU ANATAKA SERIKALI ICHUKIWE?
Wapo waliodai kuwa kama mrusha bomu yupo nje ya siasa, basi zinazofanyika ni njama nzito za kuwagombanisha wananchi na serikali yao ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kitu ambacho serikali inapaswa kufanyia kazi.
“Kuna uwezekano labda ni haya makundi ya kigaidi na waasi kama M-23 na Al-Shaabab yanayolenga kuzivuruga serikali za Afrika Mashariki kwa kuzichonganisha na wananchi wake,” alisema Mzee Minja, kada wa Chadema mjini hapa.
Baadhi ya wananchi walisema mlipuaji alilenga kuua watu wengi na matokeo yake ni kwamba licha ya watu hao wawili kufariki dunia, majeruhi waliolazwa katika hospitali mbalimbali jijini hapa na KCMC mkoani Kilimanjaro, idadi iliyothibitishwa na polisi imefikia 60.
Habari zilieleza kuwa majeruhi wanne, hali zao zilikuwa mbaya huku mtoto, Farad Jamal (7), akiwa katika hali mbaya zaidi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya KCMC.
Mbowe amesema “ tukio hili ni kubwa na lina mambo mengi, chama kitawahudumia majeruhi wote.”
Kufuatia tukio hilo, msimamizi wa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne, Jimbo la Arusha, Sipora Liana ambaye ni mkurugenzi wa jiji, alitangaza kuahirisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike juzi (Jumapili) hadi Juni 30, mwaka huu.
Liana alisema kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni kutokana na hali tete iliyojitokeza Jumamosi na kusababisha uvunjifu wa amani hivyo kwa mtazamo huo usingeweza kufanyika kutokana na hali ya usalama kuwa mdogo.
Mkuu wa Mkoa, Mulongo alisema kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo na aliwasihi wananchi waendelee na shughuli zao wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

MAJERUHI WAZUNGUMZA
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Seliani, Abdalah Alila (39) alisema kuwa akiwa katika mkutano huo majira ya saa 11.50 jioni, aliona kitu cheusi kikidondoka karibu yake na baadaye alisikia kishindo kizito.
“Ghafla nilijikuta chini na damu zikinichuruzika huku nikishindwa kutembea, nikatambaa kuomba msaada kwa watu waliokuwa wakikimbia hovyo,” alisema.

MRUSHA BOMU
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto, hali iliyozidisha vurugu.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za Jiji la Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia hovyo.
Kitendo cha watu kukimbia hovyo kuliwafanya polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi, hali ambayo ilizidisha taharuki.

BADO HOFU IMETANDA
Pamoja na viongozi kujitahidi kutuliza wananchi lakini bado hali ni tete jijini hapa kwa kuwa watu wana hofu hasa maeneo ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi huku wengine wakijitahidi muda mwingi kuwa majumbani mwao.
Wananchi waliozungumza na Uwazi kwa nyakati tofauti kuhusu tukio hilo, wamemuomba Rais Kikwete kufuatilia kwa kina matukio hayo ili maswali yote yanayoulizwa hivi sasa yaweze kujibiwa japokuwa tayari amesema  serikali itafanya kila liwezekanalo kuwasaka waliohusika na kitendo hicho ili washitakiwe.

No comments:

Post a Comment