Ndugu zangu,Uchaguzi
Mkuu wa Kenya umefuatiliwa kwa karibu sana na sisi Watanzania, ni
pamoja na wanasiasa wa vyama vya siasa; Chama tawala, CCM na wapinzani.
Lakini, nahofia, kuwa hakuna ambacho vyama hivi vyetu vya siasa vitajifunza kutoka Kenya.
Ndio,
pamoja na mapungufu ya hapa na pale, lakini Wakenya, kupitia Uchaguzi
wao wametuachia somo kubwa sana; kuwa hata Afrika tunaweza kuendesha
siasa za kistaarabu ikiwemo chaguzi Huru.
Ni kawaida kwa majirani
sisi; Kenya na Tanzania, kuoneana wivu kwenye kupiga hatua kimaendeleo.
Hakika ni wivu wa kimaendeleo tunaopaswa kuwa nao. Nikiri, safari hii,
kama Mtanzania, nimejisikia kuwaonea wivu Wakenya kwa jinsi
walivyoionyesha Afrika na Dunia kuwa nao wanaweza kuwa Taifa Kubwa;
kisiasa na kiuchumi.
Mchakato ule wa mabadiliko ya Katiba yao na hata
kufanya uchaguzi ule kwa amani na uwazi ni USHINDI mkubwa wa kimfumo.
Ni ushindi wa Wakenya wote. Kwamba Wakenya wameujaribu mfumo mpya.
Umeonyesha kuwa unafaa.
Kwa mfano, kufuatilia matokeo ya uchaguzi ule
kutoka kwenye Tume yao Huru ilikuwa ni kama ‘ burudani’ ya kisiasa.
Kila kitu kilikuwa kinawekwa wazi na kisayansi.
Si ajabu Wakenya
waliweza kusubiri matokeo kwa juma moja bila kurushiana mawe. Na hata
kama ingekuwa kusubiri kwa majuma mawili, naamini kuwa Wakenya wale
wangesubiri bila kupigana, maana, wamekuwa na imani kubwa na Tume yao
Huru ya Uchaguzi. Na hatukusia kule Kenya, habari ya watu ‘ kulinda
kura’ wala kusimama hatua mia moja kutoka kituo cha kuhesabia kwa usiku
mzima. Hiyo kazi iliachiwa Tume Huru ya Uchaguzi walioiamini.
Ndio,
Wakenya wamejifunza kutokana na ujinga wa wanasiasa wao uliopelekea
vurugu za baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007. Wengi walikufa na wengine
kupoteza makazi na mali zao. Wakaanza haraka mchakato wa kuifanyia
marekebisho makubwa Katiba yao. Wakapata Katiba Mpya 2010. Wakenya wale
wametumia gharama kubwa kwa kuitafuta amani yao. Kimsingi, tangu 2010,
Wakenya wamekuwa ‘ wakiangushiwa mabomu ya ujumbe wa amani’- Ni kila
kukicha.
Serikali yao imetumia fedha nyingi sana kufikisha ujumbe wa
amani kwa Wakenya. Sasa wanavuna walichopanda; kuwa na chaguzi huru za
amani na utulivu. Na walichokitafuta Wakenya kwa gharama kubwa, kwa
maana ya amani, sisi Watanzania tulikuwa nayo, sasa tunaipoteza wenyewe
ili baadae tuanze kugharamia kuitafuta. Ni ulimbukeni.
Kwa kupitia Katiba yao ya sasa Wakenya wameweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ukabila. Kwa namna gani?
Ona
kwenye kugombea Urais; mgombea lazima afikishe asilimia 50+1 ( Asilimia
50 na kura moja) ili aweze kutangazwa mshindi. Mgombea pia lazima
akubalike kwa asilimia 25 ya Counties zote ( Majimbo yote).
Sasa basi, kwa Kenya, Wakikuyu ni asilimia 23 ya Wakenya. Wajaluo asilimia 11.
Nyingine
zilizobaki ni za makabila mengine madogo madogo. Hivyo, ili mgombea
ushinde zaidi ya asilimia 50 una lazima ya kukubalika kwenye maeneo
mengine nje ya wigo wa kabila lako. Kwamba kula za Wakikuyu pekee kwa
Uhuru Kenyatta zisingetosha, vivyo hivyo kwa Odinga.
Utaratibu huo
unaua ukabila na kujenga vema misingi ya Utaifa. Hata kama itachukua
muda kufika mbali zaidi katika hilo lakini Wakenya wameanza kuondokana
na ukabila kwenye siasa zao, kwa kupitia Katiba.
Kwa mantiki hiyo
hiyo, Watanzania tungeweza kabisa kuondokana na siasa za udini kwa
kuweka, kwenye Katiba yetu ijayo sharti la mgombea Urais kushinda kwa
asilimia 50+1 ( Asilimia 50 jumlisha kura 1). Hilo lingewafanya
wanasiasa wetu wenye kuwania Urais na vyama vyao pia ‘ Kutia akili’.
Maana
ingekuwa na tafsiri moja kuu; kuwa mgombea na chama chenye kuendekeza
udini kisingekuwa na nafasi ya kutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wala nafasi ya kushika dola. Maana, hakuna dini hapa Tanzania
yenye idadi ya waumini wanaovuka asilimia 50 ya jumla ya Watanzania.
Kwa
maana, hiyo, muarobaini wa kumalizana na udini uko kwenye Katiba ijayo,
kama tuna nia ya dhati ya kutoka hapa tulipo. Vinginevyo, udini huu
tunaosema kuwa ni tatizo tutakuwa tunaulea wenyewe.
Hata tatizo la
siasa za ukanda nalo litapotea, maana, hakutakuwa na mgombea au chama
kitakachoweza kushinda na kutoa Urais kwa kuegemea kura za kikanda.
Hakuna kanda itakayovuka peke yake asilimia 50 ya kura zote. Chama na
mgombea kitahitaji kuungwa mkono na wapiga kura wa kanda hata zilizo nje
ya anakotoka mgombea Urais.
Vinginevyo, kama alivyotamka Uhuru
Kenyatta kwenye hotuba yake nzuri iliyojaa utaifa hivi majuzi, kuwa
katika uchaguzi waliofanya, kila kura ilikuwa ina umuhimu. Hivyo, kila
kabila lilikuwa na umuhimu. Na Uhuru Kenyatta akaweka wazi anachotaka
Serikali yake kwa kushirikiana na Wakenya kufanya ili kuitoa Kenya hapo
ilipo na kwenda mbele.
Kenyatata alimalizia na maneno matatu; Forward, Foward. Foward!- Kusonga mbele!
Ndio, Wakenya wameamua; KENYA KWANZA!
And really, The Kenyans are coming, Big Time!
Ni
ukweli, Wakenya wanakuja. Kisiasa na kiuchumi. Sisi hatujajipanga na
hatutaki kujipanga kwa dhati. CCM na wapinzani, na hata media yetu, kama
kawaida, tumerudi kwenye kucheza ‘ Kiduku’ chetu. Hatuna cha kujifunza
kutoka Kenya. Tumerudi kwenye mambo yetu ya hovyo hovyo; ni Siasa za
Mwembe Yanga na Viwanja Vya Jangwani. Siasa za kupigana vijembe. Siasa
za reja-reja- Retail politics.
CCM na wapinzani ni kama vile wapenzi
wa soka. Wanaangalia kila siku soka la majuu. Wataongea sana kuhusu soka
la majuu lilivyo bora.
Lakini, wakirudi kwenye soka lao, ni yale
yale, hawana cha kujifunza na hawataki kujifunza. Ni madudu kwenye
kuendesha vilabu na hata kufikia kununua mechi kwa kuhonga marefa,
wachezaji na viongozi. Ukisema nini hiki?
Utajibiwa; “Wewe Bongo
mpira pesa bwana!” “Mpira fitna!” Ni kama majibu ya wanasiasa, iwe wa
CCM au vyama vya upinzani. Nao watakwambia; “Wewe, Bongo siasa pesa
bwana!” “ Siasa mizengwe na fitna!”
Naam, nahofia, kuwa CCM na wapinzani hawana cha kujifunza kutoka Kenya!