NEMAYAN

NEMAYAN

ROBERT

  • THE HOODS SPICK

Thursday, March 28, 2013

UNAPOPATA FEDHA, ‘USIZITUMBUE’ KANA KWAMBA KESHO HAIPO!


Leo nataka kuzungumzia tabia ya baadhi ya watu kutumia fedha wanazozipata kwa fujo kana kwamba wameambiwa kuwa kesho wanakufa. Hakuna asiyefahamu umuhimu wa pesa, na kutokana na hilo, wengi wamekuwa wakipambana usiku na mchana kuhakikisha wanazipata.
Cha ajabu sasa, wapo ambao wanatumia nguvu na akili zao kuzitafuta fedha hizo lakini mwishowe wanazimwaga kwa matumizi yasiyo na mbele wala nyuma.
Utakubaliana na mimi kwamba wapo watu ambao leo hii wanashinda wakibeba zege, kuzibua mitaro, kubeba mizigo na kazi nyingine nzito lakini jioni wanapopata ujira hukimbilia baa na kuzitumbua kwa staili ya lete kama tulivyo.
Ninachokizungumza kipo huko mtaani, watu wanatumia pesa kama vile wana uhakika wa kuendelea kuzipata kila siku. Ndiyo maana nadiriki kusema kwamba kutumia pesa ovyo ni sawa kabisa na kujiandalia ufukara wa baadaye.
Wapo watu wengi tu ambao kwa sasa ni mafukara wa kutupwa lakini utakapojaribu kuangalia historia yao huko nyuma utagundua walikuwa na pesa nyingi ila walikuwa wakizutumia kana kwamba wanamkomoa mtu lakini leo wanaishi maisha ya kuungaunga, hawana mwelekeo.
 Sikatai kwamba matumizi ya mtu yanatokana na kipato chake na ndiyo maana mtu anayepokea mshahara wa shilingi milioni moja kwa mwezi hawezi kuwa na matumizi sawa na mtu anayepokea laki moja lakini je, kuwa na kipato kikubwa ndiyo kukufanye utumie fedha zako ovyo eti kwa sababu tu una uhakika wa kupata nyingine mwezi ujao?
Jamani tukumbuke kwamba, maisha ni kupanda na kushuka. Leo hii unafanya kazi katika kampuni ama shirika fulani lakini uwezekano wa kuwepo katika shirika hilo kwa kipindi chote cha maisha yako ni mdogo. Unaweza kuachishwa kazi wakati wowote.
Sasa kama ulikuwa unatumia ovyo pesa uliyokuwa unaipata, unatarajia nini kama siyo kuingia kwenye ufukara ambao kwa kiasi fulani ungeweza kupunguza ukali wake kama ungekuwa makini katika matumizi ya pesa zako?
Utumiaji ovyo wa pesa ni kuzitumia bila mpangalio tena wakati mwingine katika mambo ambayo si ya msingi lakini tutambue kwamba, ufujaji wa pesa hauko katika anasa tu kama vile ulevi, kuhonga na mambo mengine kama hayo, bali pia katika mambo ambayo hata yakikosekana hayawezi kuleta athari.
Tafiti mbalimbali zimeonesha kwamba, wengi ambao hutumia pesa ovyo ni athari za malezi waliyoyapata kutoka kwa wazazi wao tangu utotoni. Mzazi ndiye anayeweza kumfundisha mtoto wake kutokuwa na nidhamu katika pesa.

Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment