Stori: Francis Godwin, Iringa
“HUJAFA
hujaumbika, Mungu ana makusudi yake na yeye ni muweza wa yote kwani
ndiye aliyeumba mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na
visivyoonekana.” Hiyo ni kauli ya mzazi wa mtoto Zawadi Godfrey
Mwingune aliyezaliwa akiwa na macho matatu na kichwa mfano wa uyoga.
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita mama mzazi wa mtoto
Zawadi, Marthar Kitago (28) mzaliwa wa Kijiji cha Kidegembye Lupembe
wilayani Njombe mkoani Njombe alisema kuwa hadi sasa anamwachia Mungu
ambaye ndiye amempa zawadi ya mtoto huyo.
“Jumapili Januari 13,
mwaka huu nilishikwa na uchungu nikakimbizwa katika Kituo cha Afya cha
Kidegembye ambako sikukaa nikahamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Njombe
Kibena ambako nilifanyiwa upasuaji na kubahatika kumpata mtoto huyu.
“Niliogopa sana baada ya kuonyeshwa mtoto wangu
jinsi
alivyo ila nilipiga moyo konde kwa kuwa ni damu yangu, tukampa jina la
Zawadi, tukiwa na maana ni kutoka kwa Mungu,” alisema mama huyo wa
watoto watatu.
Baba wa mtoto huyo, Godfrey Mwingune anayeendesha
maisha yake kwa kilimo alisema kuwa hali ya afya ya mtoto huyo si nzuri
kwani mbali ya kuzaliwa na kilo 4 na nusu, bado ana tatizo la uvimbe
katika paji lake la uso unaofanana na umbo la uyoga pia kichwani kuna
kovu kubwa kama ncha mbili hivi ambalo linatoa usaha mwingi.
Akaongeza
kuwa katika jicho lake la kushoto kwa juu kuna jicho la pili na
kufanya mtoto huyo kuwa na macho matatu ambapo madaktari wamemshauri
ampeleke katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Amesema
fedha zinazotakiwa ili mwanaye apatiwe tiba ni shilingi 1,500,000 na
amewashukuru wakazi wa Isimani ambao wamemchangia shilingi 300,000
kwani yeye hana uwezo.
Walioguswa na habari hii wanaweza kumchangia mtoto huyu kupitia namba 0754 026 299 au
0712 750 199- Mhariri.
No comments:
Post a Comment